Advertisements

Monday, February 8, 2016

MHIFADHI NGORONGORO ADAKWA KWA UJANGILI

Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, Iddi Mashaka, ambaye pia ni afisa intelijensia wa hifadhi hiyo, amekamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio la utunguaji wa helkopta namba 88HF na kusababisha kifo cha rubani wake, Rogers Gower, raia wa Uingereza.

Imeelezwa mashaka amekuwa kinara mkubwa wa ujangili katika hifadhi mbalimbali zilizopo kanda ya ziwa kwa kutoa ushirikiano kwa majangili wenzake pamoja na kuwaazimisha silaha za kufanyia ujangili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, kamanda wa polisi mkoani Simiyu, Lazaro Mambosasa, amesema mtuhumiwa huyo ni mwajiriwa wa hifadhi hiyo ya Ngorongoro.

Kamanda Mambosasa amesema jitihada zilizofanywa na jeshi la polisi mkoani Simiyu, zikiongozwa na mkuu wa upelelezi, Jonathan Shana, zimeendesha msako maalum uliowashirikisha askari wa vyeo mbalimbali, kikosi kazi na askari wanyamapori pamoja na wananchi, wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wenzake nane walioshiriki katika tukio hilo.

Kamanda amewataja watuhumiwa hao ni Shija Mjika, Njile Gonga, Masasi Mandago, Mwigulu Kanga, Mapolu Njile, Dotto Huya, Mange Balum na Dotto Pangali ambao wamedaiwa kuhusika na tukio hilo la kikatili lililokatisha maisha ya rubani wa helikopta iliyokuwa ikifanya doria eneo la Gululu ndani ya hifadhi ya Maswa katika kitalu cha mwekezaji Mwiba holding ltd.

Vile vile amemtaja Dotto Pangali ndiye aliyefanikiwa kutungua ndege hiyo kwa kutumia bunduki aina ya rifle namba 7209460 CAR na 63229, alipohojiwa alikiri bunduki hiyo ni mali ya Mange Magima.

Hata hivyo, kamanda Mambosasa amesema katika tukio hilo, Shija, Njile na Masasi Mandago waliweza kuonyesha ushirikiano wa karibu kwa kuwaonyesha meno mawili ya tembo yenye uzito wa kilo 31 waliyokuwa wameyaficha chini ya daraja kijiji cha Itaba.

Ameongeza mbali na tukio hilo la kukamatwa watuhumiwa hao, meno mawili ya tembo, jeshi la polisi waliweza kukamata bunduki 29 na risasi 141 ambazo wamiliki wake wamekamatwa kwa ajili ya mahojiano kutokana na kukiuka masharti ya umiliki wa silaha hizo.

4 comments:

Anonymous said...

wazungu kulinda hifadhi zetu? tumeishiwa walinzi au vipi?

Anonymous said...

Ndio wazungu kulinda hifadhi zetu kwa sababu sisi wenyewe ni watu wa hovyo hatujui thamani ya hizo hifadhi tupo tayari tuwamalize tembo wote,Faru wote,Nyati wote yaani hatusomi makosa ya wenzetu,Msumbiji wukuwa na wanyamapori kuliko Tanzania leo unawatafuta kwa helicopter. Marekani walikuwa na Nyati(American Buffalo) wamezagaa kila kona ya marekani leo unawatafuta hata hapo nyumbani kuna baadhi ya wanyamapori katika hifadhi fulani unawatafuta. Sasa leo mhifadhi intelinjisia mtu ambae ana siri za mikakati yote ya kiuhifadhi na ulinzi wa wambuga zetu ndie jangili mkuu kama si upumbavu kitu gani? Siku zote tunasema mvunja nchi ni mwananchi mwenyewe sio mgeni. Huyo ndugu mhifadhi inabidi jangili inabidi apewe adhabu ya mfano ili iwe fundisho kwa wengine. Kwanza achunguzwe vya kutosha kwani hakika atakuwa na wenzake miongoni mwa wafanyakazi wenzake wanashirikiana katika uhalifu. Achunguzwe kama atakuwa ana mali alizozipata kwa kazi yake ya ujangili zifilisiwe na kurejeshwa katika mfuko wa hifadhi . Hongereni sana wahusika waliofanikisha kukamatwa kwa wale wote waliohusika kuiangusha ile helicopter na kupoteza maisha ya yule rubani hakika lilikuwa tendo la kusikitisha na kukatisha tamaa.

Anonymous said...

Ujangili na mauaji ya wanyama pori ni vigumu kuisha kwa sababu wahusika wakubwa ni baadhi ya wafanyakazi wa mbuga za wanyama pori na hata sio ajabu waliokuwa viongozi wa juu wanahusika. Hayo ni majipu makubwa yanayobidi kupasuliwa.

Anonymous said...

Kama walinzi wenyewe ndio majangili, what do you excpect?