Advertisements

Sunday, November 23, 2014

`Werema jiuzulu`

  Wabunge CCM washinikiza kuiokoa serikali kashfa ya Escrow
  Atia ngumu, adai hadi mtu aliyemwita ``bwana mkubwa`` pia anaijua
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema

Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, kujiuzulu ili kuisafisha serikali dhidi ya kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ya uchotwaji wa Sh. bilioni 306 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Ushauri wa kumtaka Jaji Werema ajiuzulu ulitolewa na wabunge; Kangi Lugola (Mwibara-CCM) na Deo Filikunjombe (Ludewa-CCM), katika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa Chama hicho, kilichofanyika mjini hapa juzi.

Lugola alihudhuria kikao hicho kama mwalikwa kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) badala ya Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk Mohammed, ambaye ni mpinzani kutoka Chama cha Wananchi (CUF).

Kwa upande wake, Filikunjombe alihudhuria kikao hicho kama mwalikwa kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), badala ya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe ambaye ni mpinzani kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho kinaeleza kuwa Lugola na Filikunjombe kwa nyakati tofauti, walimtaka Jaji Werema kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, sababu iliyotolewa na wabunge hao ni kwamba, kashfa hiyo imeichafua serikali, hivyo kujiuzulu kwa Jaji Werema kutaipa nafuu.
Hata hivyo, chanzo hicho kinaeleza kuwa Jaji Werema hakukubaliana na ushauri huo.

Badala yake, alinukuliwa akisema kuwa kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow hakuna kiongozi yeyote serikalini asiyeijua na kwamba, viongozi wote wanaijua hadi mtu aliyemwita "bwana mkubwa" pia anaijua.

Alipoulizwa na mwandishi, Katibu wa Kamati ya Uongozi wa Wabunge hao, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, alisema hakuna kikao chochote kilichofanyika.

Akaunti hiyo ilifunguliwa kutokana na kutoelewana kuhusu gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika uamuzi wake wa Februari 2014, ilitoa hukumu kuonyesha kwamba, Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL.

Kwa uamuzi huo, ni dhahiri kuwa fedha zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti hiyo zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco.

Hiyo ni baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali. Lakini badala yake, fedha hizo zilitoweka ghafla kwenye akaunti hiyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

5 comments:

Anonymous said...

Kujiuzulu tu haitoshi na hizi fedha hakuzila yeye peke yake kuna mlolongo mrefu tunataka ushughulikiwe. Swala hapa sio kuiokoa CCM tunaangalia maslahi ya Taif kwa ujumla na wala sio maswala ya kisiasa kabisa siasa iwekwe mbali kwanza na hizi fedha zirudishwe haraka. Tuacheni mchezo wa kijinga!!

Anonymous said...

Well said mdau no 1 hapo juu. Was he a judge, they should review all his judgements, there is a possiblity innocent people were jailed. Jamani, hivi watu wanakula hela za uma bila hata kutuonea huruma, hospitali no dawa, shule hazina madawati, hivi tunaenda wapi.

Anonymous said...

It will be very interesting to see the names of people involved in this saga, I cannot wait. Jamani, nchi inaliwa utafikiri hakuna kesho,

Anonymous said...

Hawq jamaa warudishe pesa.na huu uwe ndio mwanzo

Anonymous said...

Jamani hawa sio watu lazima hatua kali ichukuliwe...jasho la watanzania. Hakuna alie lala tena. Aibu viongozi gani wamemaliza nchi.