Advertisements

Sunday, November 16, 2014

MTOTO ANAYEDAIWA KUGEUKA NYOKA AYEZUA KIZAAZAA HUKO GEITA

Katioka gazeti la Mwananchi la leo kuna habari ya mtoto mchanga mwenye umri wa miezi minne amezua kizaazaa cha aina yake, baada ya kuwapo taarifa kwamba mara kadhaa umbo lake limekuwa likigeuka na kuwa nyoka na mwili wake ukiendelea kudhoofu kutokana na kukataa kunyonya maziwa ya mama yake.

Mtoto huyo (jina lake tunalihifadhi kwa sasa), wiki iliyopita alivuta umati wa wakazi wa Kijiji cha Nkome mkoani Geita ambao walifurika ndani na nje ya Kanisa la AICT Nkome, lililopo kijiji hapo, kushuhudia maombi ambayo alikuwa akifanyiwa ili kumkomboa katika kile kilichotafsiriwa kuwa ni mateso dhidi yake.

Ilikuwa saa 4.00 asubuhi Jumamosi, Novemba 8 mwaka huu wakati mtoto huyo alipofikishwa katika kanisa hilo na kuanza kufanyiwa maombi na sababu ya hatua hiyo ikielezwa kuwa ni kutokana na kuwa na umbo la nyoka na kwamba matendo yake yanaashiria kwamba mwenye asili ya nyoka ndani ya roho yake.


Mtoto huyo alifikishwa kanisani hapo na mama yake mzazi, Sarah Silasi wakitokea Kijiji cha Ichile, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, ambako alikimbia matukio yanayohusishwa na ushirikina.

Mmoja wa wazee wa kanisa hilo la AIC Nkome, Mathew Misana anasema: “Alikuwa anatoa ulimi mithili ya nyoka, mwendo wake anapolala alijizungusha kama nyoka na hata alipojikunja mwili wake ulikuwa kama unavyoona nyoka.”

Misana anasema matukio hayo na mengine kadhaa yakiwamo ya ngozi ya mtoto huyo kuwa nyeusi kama ya nyoka aina ya chatu, yaliwalazimisha ndugu na jamaa zake wakiongozwa na mama mzazi kutaka aombewe.

“Ngozi yake kuonekana kama ya mzee huku macho yake yakionekana kuwa makubwa na kichwa chake kuwa na umbo la nyoka pamoja na miguu, baada ya kuona hali hii tukaihusisha na mambo ya kishirikina na kuamua kuanza maombi,” alisisitiza.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya maombi kuanza, taarifa za kuwapo kwa aina hiyo ya mtoto zilisambaa haraka na kusababisha umati mkubwa wa watu kujaa ndani ya kanisa hilo ambalo ni boma kwa maana kwamba ujenzi wake bado unaendelea.

“Watu wengi walijaa na wengine wakawa wanapanda juu ya miti na juu ya boma wakati mwingine matofali yalianguka. Hewa ikapungua na usalama ukawa mdogo kwani watu walisukumana wakitaka kushuhudia,” anasema Misana.

Baada ya watu kuwa wengi, uongozi wa kanisa uliomba msaada wa Polisi wa Kituo cha Nkome ambao walifika kanisani hapo na kushauri mtoto huyo aonyeshwe ili watu waweze kuridhika kwamba hakuwa amegeuka kuwa nyoka.

Uongozi wa kanisa ulifanya hivyo lakini mwonekano wa mtoto huyo ulisababisha watu kuongezeka badala ya kupungua na hapo ndipo polisi walipoelekeza mama wa mtoto huyo ambebe na kuondoka naye hadi kituoni.

Mwinjilisti wa kanisa hilo, Emmanuel Misungwi anasimulia: “Tumeshudia vitu visivyo vya kawaida wakati tunafanya maombi na wakati tunaendelea na huduma, mama wa mtoto Sarah alianguka akaanza kuongea juu ya mtoto kwa nguvu ya mapepo.”

Anasema hali hiyo iliwavuta watu wengi kiasi cha usalama wa mtoto kuwa mdogo, ndipo walipoamua kuomba msaada wa ulinzi kutoka polisi.

“Ilibidi polisi waingilie kati, walimchukua mtoto na kuondoka naye na kuwaridhisha wananchi kwa kumwonyesha hadharani ili kila mtu aone kama kweli ni nyoka kama uvumi ulivyokuwa umeena au la,” anasema Misungwi.

Kituo cha polisi

Baada ya mama huyo na mwanaye kufikishwa polisi, umati wa watu ulihamia katika kituo hicho na kuwafanya askari kufanya kazi ya ziada kuwaondoa watu waliokuwa wamekusanyika katika eneo hilo.

Licha ya wananchi kufukuzwa waliendelea kun’gang’ania kukaa katika kituo hicho, hali ambayo ilisababisha polisi kumwondoa mwanamke huyo kwa kificho na kumpeleka nyumbani kwa mchungaji wa kanisa hilo, Mchungaji Mkuu wa Kanisa hilo Jonh Marko.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nkome, Charles Belenge alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa hali hiyo imesababisha vurugu wakati wa maombi.

“Nikweli tukio hilo lipo la kudai mtoto anabadilika kuwa nyoka, kwa kweli limetupa shida kwani hali ya utulivu katika kijiji ilibadilika kwa muda, lakini tumejitahidi kufanya udhibiti,” anasema Belenge.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba walikuwa wakilifanyia uchunguzi wa kina.

“Haya mambo ndiyo yanasababisha mauaji ya mapanga, hivyo kama Jeshi la Polisi tutafuatilia kujua kwa kina ili lisije kusababisha madhara ya mauaji ya kukatana kwa mapanga,” alisema Konyo.

Alihusisha tukio hilo na uelewa mdogo wa wazazi na wachungaji waliokuwa wakifanya maombi na kwamba mtoto huyo huenda alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya utapiamlo, tofauti na mawazo kwamba tatizo ni nguvu za giza.

“Kazi tunayoifanya kama Jeshi la Polisi ni kuweka ulinzi kwa kuzuia wasifanye maombezi eneo la kanisa hilo ambalo kiukweli liko wazi sana kwani usalama utakuwa mdogo pia tuombe wanaohusika wampeleke mtoto hospitali,” alisema Konyo.

Mashuhuda wa maombi
Misana anasema wakati wakifanya maombi mtoto huyo alikuwa hatoi sauti isipokuwa alikuwa anatoa ulimi kama ufanyavyo nyoka na kwamba ulimi huo ulikuwa mrefu mpaka shingoni pamoja na macho yake kuwa makubwa.

Mashuhuda wengine walisema kuwa waliona mtoto huyo akigeuka kimaajabu na kuwa na maumbo mithili ya nyoka na baadaye kurudi katika umbo la binadamu.

“Mimi nimeona wakati anaombewa alikuwa anatoa ulimi kama nyoka, alikuwa anasimamisha kichwa na kutoa ulimi hadi unagusa shingo halafu tumbo, miguu na kiuno vilizunguka,” anasimulia mkazi wa Nkone, Shaban Masembe.

Naye Neema Masatu anasema: “Niliambiwa Kanisa la AIC kuna mtoto anabadilika kuwa nyoka anafanyiwa maombi ikabidi nije nijionee, nimefika hapa nikakuta kweli watu wamejigawa makundi mawili; wengine wanamuombea mama wa mtoto na wengine mtoto.”

Masatu anafafanua kuwa alichokiona si nyoka isipokuwa ameona mtoto huyo akiwa anatembea kama nyoka, anajikunja miguu inagusa shingo kisha kichwa anakisimamisha kama nyoka na kutoa ulimi mrefu na mdomo na macho yake yalikuwa yanakuwa makubwa.

Naye Pili Nyachimb’huga anasema: “Sijaona, watu walikuwa wengi nimefika hapa hata sikuweza kumuona ila watu wanasema alikuwa mtu anayefanana na nyoka, alikuwa anaachama kama nyoka na kwamba alikuwa anatanuka mwili wake unakuwa mkubwa”.

Ni ipi historia ya mtoto huyu?
Wiki ijayo gazeti la Mwananchi Jumapili litachapisha muendelezo

No comments: