Advertisements

Wednesday, October 22, 2014

CHETI CHA KUZALIWA CHA MISS TANZANIA KILITOLEWA SIKU 4 KABLA YA KAMBI YA WASHIRIKI WA MISS TANZANIA KUANZA


Mkurugenzi wa kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga (kulia) akionyesha cheti cha kuzaliwa cha Miss Tanzania 2014, Sitti Mtevu kilichoandikwa amezaliwa mwaka 1991 wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha: Omar Fungo


Sakata la umri halisi wa mrembo mpya wa Tanzania mwaka huu 'Redd's Miss Tanzania 2014', Sitti Mtemvu bado linaendelea kuchukua sura mpya baada ya mshindi huyo wa taji la taifa kuwasilisha cheti cha kuzaliwa ambacho kimetolewa siku nne kabla ya kambi ya washiriki wa shindano hilo kuanza huku akishindwa kuikana ama kuikubali hati yake ya kusafiria na leseni ya udereva zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga, alisema jana kuwa cheti kilichowasilishwa na Sitti kinaonyesha amezaliwa Mei 31, 1991, Temeke.

Lundenga alisema kanuni na taratibu za Miss Tanzania zinaeleza kuwa mshiriki wa shindano hilo anatakiwa awe na umri wa kuanzia miaka 18 na si zaidi ya 24, hivyo Sitti alikuwa na kigezo cha kushiriki kinyang'anyiro hicho.


Cheti hicho kipya kilichoonyeshwa jana jijini kina namba 1000580309 kikitaja jina la baba yake ni Abbas Mtemvu Zuberi ( Mbunge-Temeke) na mama yake ni Mariam Nassor Juma ambaye ni diwani wa Temeke.

"Suala la umri wa mshiriki, Miss World 'flexibility' wana ruhusu mshiriki wa kuanzia miaka 17 na hata wenye miaka 25 na 26 wameshawahi kushiriki shindano hilo la kimataifa, ingawa Tanzania hatujawahi kupeleka mwakilishi mwenye umri wa miaka 25," alisema Lundenga.

Aliwataja warembo wengine ambao walipeleka vyeti vya kuzaliwa vilivyotolewa hivi karibuni na kuruhusiwa kushiriki shindano la mwaka huu ambalo lilifanyika Oktoba 11 kwenye Ukumbi wa Mlimani City kuwa ni pamoja na Lilian Timothy ambaye cheti chake kilitolewa Oktoba 3 na Naba Magambo cha Agosti 5, mwaka huu.

KUVULIWA TAJI
Kuhusiana na suala la Sitti kuvuliwa taji hilo, Lundenga, alisema kuwa kwa sasa wanaendelea na uchunguzi wa suala hilo na endapo itabainika Sitti alidanganya umri atachukuliwa hatua ingawa hakuwa tayari kuweka wazi adhabu atakayopewa.

Lundenga alisema Kamati yake kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) watakutana na kujadili hatma ya mrembo huyo.

"Kanuni zetu hazisemi kitu kuhusiana na suala hilo, kwa sababu halijawahi kutokea tangu 1994 tulipoanza, ila tutashirikiana na Basata ili kujua maamuzi tutakayoyafikia," alisema Lundenga.

Mratibu huyo alieleza kusikitishwa na kuona suala na taarifa za mrembo huyo kusambazwa katika mitandao ya kijamii na kufafanua kwamba limehusishwa na siasa, hasa kutokana na baba yake, Abbas Mtemvu, kuwa Mbunge wa Jimbo la Temeka (CCM).

Pia alisema kamati inakanusha taarifa za Sitti kuwa na mtoto na kama kuna mtu mwenye ushahidi wa hilo aliwasilishe katika kamati na litafanyiwa kazi mara moja.

Kuhusu zawadi zilizotolewa kwa mshindi huyo ambapo ukumbini alikabidhiwa hundi ya Sh. milioni 10 na kudaiwa ilikuwa ni 'kanyaboya', alisema jambo hilo halina ukweli wowote.

"Napenda pia kuzungumzia suala la rushwa, sisi kamati tumezungumzwa sana eti tumepokea rushwa na Mtemvu Foundation imehusika, si sahihi, majaji wa shindano hili walikuwa tisa kati ya 15 ambao majina yao tuliyapeleka Basata, hapo wapo na wadhamini, je mdhamini anaweza kukubali kupokea rushwa ili kumpa alama mrembo," Lundenga aliongeza.

Kuhusiana na Sitti kuzungumza lugha ya Kifaransa wakati akijibu swali, alisema kwamba si kosa kwa sababu ni lugha ambayo aliijaza pia kwenye fomu zake na ni moja ya mbinu alizotumia kuwashawishi majaji na alifanikiwa kwa hilo.

Lundenga alisema mrembo huyo hana shahada ya uzamili kama ilivyodaiwa na kutaja kiwango chake cha elimu ni ngazi ya shahada ya Uhusiano wa Kimataifa aliyosomea katika Chuo Kikuu cha North Texas kilichoko jijini Dallas, Marekani.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Kweli mambo ya rushwa yamekubuhu Tanzania/Africa, they know what they need to do,but nobody is willing to do it. Why are they wasting time beating around the bush! Birth certificate doesn't mean sh*t in Bongo...This is what they need to do:
1)Find out where she went to primary school (Original records should be there)-She was 6yrs old in 1997.
2)Verify with her primary school classmates they should be around the same age +/-1.
3)Verify where she went to high school.

This chronological of events can't lie...Oops I might be wrong.. watu watanunuliwa ku-verify mambo yote...

~CK