Advertisements

Tuesday, August 26, 2014

NYERERE ALIVYOLIZA WATU UWANJANI-2


MWALIMU Julius Nyerere baada ya kustaafu urais mwaka 1985, aliondoka jijini Dar na kurejea moja kwa moja Butiama, mkoani Mara. Tulieleza jinsi alivyoliza watu Uwanja wa Ndege wa Zamani (Terminal One), waliokwenda kumuaga.

Baada ya kupanda ndege safari ilianza kuelekea kwao. Mwalimu Nyerere alipoingia kijijini Butiama hakutaka kwenda nyumbani kwake moja kwa moja. Badala yake alikwenda nyumbani kwa kaka yake, Chifu Edward Wanzagi Nyerere.

Mwalimu alikuwa na kawaida ya kumuenzi kaka yake huyo kutokana na ukweli kuwa ndiye aliyemsomesha na kumtunza hadi alipoanza kujitegemea.

Tofauti na walivyo watu wengine waliopata kuwa katika nafasi kama yake, Mwalimu aliishi maisha ya kawaida sana, ambayo hayakumtofautisha na mwanakijiji wa Butiama.
Maisha yake kijijini yalikuwa na mpangilio maalum. Kila siku asubuhi na jioni, kabla ya kuendelea na kazi zake shambani, ilikuwa ni lazima kwake kwenda kusali kanisani.

Baada ya kutoka kanisani asubuhi alikuwa akipata kifungua kinywa, mara nyingi ikiwa ni chai au uji, vilivyochanganywa na karanga. Aghalabu vitafunio vyake vilikuwa ni mihogo au viazi vilivyochemshwa. Ilikuwa ni mara chache kula mkate au maandazi.

Haikuwahi kutokea Mwalimu akapata kifungua kinywa akiwa peke yake. Mara zote alikuwa akishiriki mlo huo na wajukuu, majirani au wageni.

Alikuwa ni mkulima na mfugaji, akiwa na mashamba yenye ukubwa zaidi ya eka 90. Alikuwa akilima mahindi, karanga, mihogo, pamba, nyonyo, mtama, ulezi, viazi na maharage. Alikuwa pia mfugaji, akifuga ng’ombe, mbuzi, kuku na nguruwe.

Kwa kawaida alikuwa akifanya kazi shambani hadi mchana, kisha hurejea nyumbani kupata chakula. Baada ya kula alikuwa akipumzika kidogo na kurudi shambani saa 10 au 11 jioni.
Nyumba yake ndogo iliyojengwa kwa matofali ya zege na mawe, ipo juu ya mlima, mahali ambako aliishi baba yake, Chifu Burito.

Mazingira yanayoizunguka nyumba hiyo ni ya asili, ingawa waweza kuona vifaa vya teknolojia ya kisasa. Ni ya asili kwa sababu ni mahali ambapo wapo wanyama aina ya ngedere na pimbi, ambao hupanda kwenye nyumba na kusogea kwenye jiko ili kupata mabaki ya chakula.

Sehemu ya nje, ambako hupokelea wageni, kuna kibanda kilichojengwa juu ya mawe. Hapo kuna meza yenye bao. Mwalimu alikuwa ni mpenzi wa mchezo wa bao. Alikuwa akicheza na wageni, ndugu, marafiki na jamaa zake waliomtembelea.

Kusini na mashariki ya kibanda hicho kuna vihenge vya kuhifadhia nafaka. Ilikuwa ni kawaida kuwakuta watu kwenye vihenge hivyo, ambao walikuwa na ukosefu wa chakula. Walikuwa wakipewa chakula kulingana na maelekezo ya Mwalimu au yeyoye aliyepewa dhamana hiyo.

Upande wa mashariki kuna makaburi ya ndugu zake. Kuna kaburi kubwa lililojengwa kwa saruji. Hilo ndilo kaburi la baba yake. Sambamba na kaburi hilo kuna kaburi la mama yake, Mugaya wa Nyang’ombe aliyefariki dunia mwaka 1997, akiwa na umri unaokadiriwa kuzidi miaka 100.

Kwa hiyo, Mwalimu alikuwa akiishi katika mazingira ya kawaida, ya kijijini, akiwa amezungukwa na wananchi wengine wa kawaida. Bila shaka kuna mengi ambayo Watanzania wataendelea kujifunza kutokana na maisha yake ya kawaida.

GPL

No comments: